Date: 
10-04-2026
Reading: 
1 Wakorintho 15:35-49

Hii ni Pasaka;

Ijumaa asubuhi tarehe 10.04.2026

1 Wakorintho 15:35-49

35 Lakini labda mtu atasema, Wafufuliwaje wafu? Nao huja kwa mwili gani?

36 Ewe mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa;

37 nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au nyingineyo;

38 lakini Mungu huipa mwili kama apendavyo, na kila mbegu mwili wake.

39 Nyama yote si nyama moja; ila nyingine ni ya wanadamu, nyingine ya hayawani, nyingine ya ndege, nyingine ya samaki.

40 Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali.

41 Kuna fahari moja ya jua, na fahari nyingine ya mwezi, na fahari nyingine ya nyota; maana iko tofauti ya fahari hata kati ya nyota na nyota.

42 Kadhalika na kiyama ya watu. Hupandwa katika uharibifu; hufufuliwa katika kutokuharibika;

43 hupandwa katika aibu; hufufuliwa katika fahari; hupandwa katika udhaifu; hufufuliwa katika nguvu;

44 hupandwa mwili wa asili; hufufuliwa mwili wa roho. Ikiwa uko mwili wa asili, na wa roho pia uko.

45 Ndivyo ilivyoandikwa, Mtu wa kwanza, Adamu, akawa nafsi iliyo hai; Adamu wa mwisho ni roho yenye kuhuisha.

46 Lakini hautangulii ule wa roho, bali ule wa asili; baadaye huja ule wa roho.

47 Mtu wa kwanza atoka katika nchi, ni wa udongo. Mtu wa pili atoka mbinguni.

48 Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni.

49 Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni.

Yesu mfufuka kaa pamoja nasi;

Mtume Paulo katika somo la asubuhi hii anaandika juu ya kufufuka kwa Kristo, kufufuliwa kwa mwili, na mwili wa ufufuo. Mtume Paulo anawaondoa hofu watu wa Kanisa la Korintho, akiwaambia kwamba ufufuo wa wafu upo. Anasema Mungu aliyewapa wanadamu mwili, ndiye huyo huyo atakayewafufua waliokufa. Paulo anachokazia ni kuwa kufa ni lazima, lakini baada ya kufa kuna ufufuo.

Jambo la muhimu hapa ni kuwa Kristo alifufuka kaburini akashinda mauti. Nasi mwisho wetu katika safari ya imani ni kifo, ambapo mwili wetu unazikwa kwa tumaini la ufufuo na mwili mpya, tayari kwa uzima wa milele. Tutaufikia ufufuo kwa kutembea na Yesu mfufuka. Amina

Ijumaa njema

Heri Buberwa