Date: 
20-04-2026
Reading: 
Yohana 10:1-6

Hii ni Pasaka;

Jumatatu asubuhi tarehe 20.04.2026;

Yohana 10:1-6

1 Yesu aliwaambia, Amin, amin, nawaambieni, Yeye asiyeingia mlangoni katika zizi la kondoo, lakini akwea penginepo, huyo ni mwivi naye ni mnyang'anyi.

2 Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo.

3 Bawabu humfungulia huyo, na kondoo humsikia sauti yake; naye huwaita kondoo wake kwa majina yao, na kuwapeleka nje.

4 Naye awatoapo nje kondoo wake wote, huwatangulia; na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake.

5 Mgeni hawatamfuata kabisa, bali watamkimbia; kwa maana hawazijui sauti za wageni.

6 Mithali hiyo Yesu aliwaambia, lakini wao hawakuelewa na mambo hayo aliyowaambia.

Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo;

Yesu anajitambulisha kama Mchungaji mwema, ambaye huwaita kondoo wake kwa majina yao na kuwapa malisho. Kondoo huijua sauti yake, naye huwajua kondoo wake. Mchungaji wa kondoo huingia kwa kupitia mlangoni mwa zizi, asiyepita hapo ni mwizi. Yaani Yesu alikuwa anasema kwamba anawachunga kondoo wake kwa njia sahihi, njia ya wokovu.

Ilikuwa vigumu sana kwa Yesu kueleweka kwamba yeye ndiye Mchungaji mwema. Ukiendelea kusoma unaona kuwa wapo ambao hawakuamini, hadi kusema ana pepo!

Yohana 10:20-21

20 Wengi wao wakasema, Ana pepo huyu, tena ana wazimu; mbona mnamsikiliza?
21 Wengine wakasema, Maneno hayo siyo ya mtu mwenye pepo. Je! Pepo aweza kuwafumbua macho vipofu?

Lakini Yesu alisisitiza kwamba yeye ni Mchungaji mwema, ambaye huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Ni kweli, maana katika majira haya ya Pasaka tunakumbuka alivyoutoa uhai wake kwa ajili yetu. Katika yote tufanyayo, tumtazame Kristo aliye Mchungaji mwema kwa ajili ya wokovu wetu. Amina

Uwe na wiki njema

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com