Date: 
21-05-2026
Reading: 
Marko 10:46-52

Alhamisi asubuhi tarehe 21.05.2026

Marko 10:46-52

46 Wakafika Yeriko; hata alipokuwa akishika njia kutoka Yeriko, pamoja na wanafunzi wake, na mkutano mkubwa, mwana wa Timayo, Bartimayo, yule mwombaji kipofu, alikuwa ameketi kando ya njia.

47 Naye aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema, Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu.

48 Na wengi wakamkemea ili anyamaze, lakini alizidi kupaza sauti, Mwana wa Daudi, unirehemu.

49 Yesu akasimama akasema, Mwiteni. Wakamwita yule kipofu, wakamwambia, Jipe moyo; inuka, anakuita.

50 Akatupa vazi lake, akaruka, akamwendea Yesu.

51 Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona.

52 Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.

Mungu utusikie katika kuomba kwetu;

Jumapili iliyopita tulitafakari juu ya Yesu kuwaponya vipofu wawili waliokuwa wameketi kando ya njia. Somo lilitoka katika Injili ya Mathayo. Habari hiyo inaandikwa pia katika Injili ya Marko ambalo ndilo somo la leo. Marko anamtaja kipofu mmoja, kwa jina Bartimayo ambaye aliposikia Yesu anapita aliita kwa sauti bila kuchoka akiomba rehema. Yesu akamponya, akaona mara.

Wakati Bartimayo anamuita Yesu, watu walimzuia. Lakini walivyoendelea kumzuia, yeye ndivyo alizidi kumuita Yesu. Yesu alimsikia, Bartimayo akasema nataka nipate kuona, Yesu akamwambia Imani yako imekuponya. Kwa hiyo Bartimayo alimuita Yesu bila kuchoka, kwa Imani. Nasi tuombe bila kuchoka, kwa imani, Mungu yuko tayari kusikia maombi yetu. Amina

Siku njema

 

Heri Buberwa