Date: 
18-06-2026
Reading: 
Waefeso 2: 11-17

Alhamisi asubuhi; 18.06.2026

Waefeso 2:11-17

11 Kwa ajili ya hayo kumbukeni ya kwamba zamani ninyi, mlio watu wa Mataifa kwa jinsi ya mwili, mnaoitwa Wasiotahiriwa na wale wanaoitwa Waliotahiriwa, yaani, tohara ya mwilini iliyofanyika kwa mikono;

12 kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani.

13 Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.

14 Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga.

15 Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani.

16 Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba.

17 Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu.

Yesu ni mlango wa kuingia mbinguni;

Jana asubuhi tuliona Paulo akiwaandikia watu wa Efeso jinsi Yesu alivyowabadilisha toka maisha ya zamani. Leo asubuhi anaendelea kuwaambia kuwa walikuwa watu wa mataifa bila Kristo na kufarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio na ahadi ya Mungu. Lakini anasema wamekuwa karibu kwa damu yake Kristo. 

Paulo anasema kwamba Kristo ndiye Mwokozi wa wote. Anawataka watu wa Efeso kufahamu kwamba wokovu aliouleta Kristo ulikuwa kwa ajili ya wote. Anawaondoa shaka, kwamba hata wao wameokolewa na Yesu Kristo. Hata sisi tumeokolewa na Yesu Kristo. Tumshike yeye aliye mlango wa kuingia mbinguni. Amina

Siku njema

Heri Buberwa