Date: 
03-02-2026
Reading: 
Mathayo 16:13-18

Jumanne asubuhi tarehe 03.02.2026

Mathayo 16:13-18

13 Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?

14 Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.

15 Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?

16 Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.

17 Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.

18 Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.

Neema ya Mungu yatuokoa;

Sura ya 15 ya injili ya Mathayo mwishoni tunasoma Yesu akilisha watu elfu nne kwa mikate saba na samaki wachache. Katika sura ya 16 Mafarisayo na Masadukayo wanamuomba Yesu awaoneshe ishara itokayo mbinguni. Yesu anawaita wanafiki! Aliachana nao akaondoka, akaenda na wanafunzi wake ng'ambo. 

Huko ng'ambo Yesu akawaambia wanafunzi kuwa makini na chachu ya Mafarisayo, yaani kuepuka mafundisho yao.

Ndipo katika somo la leo asubuhi hii, baada ya ishara na mafundisho yote anawauliza wanafunzi wake kuwa watu husema yeye ni nani? Alipewa majibu kadhaa, lakini Simoni Petro alimwambia kwamba yeye (Yesu) ni Kristo, mwana wa Mungu aliye hai.

Simon Petro alitambua na kusema moja kwa moja kuwa Yesu ndiye Kristo. Yesu Kristo ndiye mwokozi wa ulimwengu, aliyeiendea njia ya mateso kwa ajili ya wokovu wetu. Yaani kwa kifo chake tumeokolewa bure, kwa neema. Kumbe tukae katika kristo, maana ndiye mwenye hatma yetu. Amina

Jumanne njema

 

Heri Buberwa