Alhamisi asubuhi tarehe 05.02.2026
Mathayo 20:1-16
1 Kwa maana ufalme wa mbinguni umefanana na mtu mwenye nyumba aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri wakulima awapeleke katika shamba lake la mizabibu.
2 Naye alipokwisha kupatana na wakulima kuwapa kutwa dinari, aliwapeleka katika shamba lake la mizabibu.
3 Akatoka mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi;
4 na hao nao akawaambia, Enendeni nanyi katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki nitawapa. Wakaenda.
5 Akatoka tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile vile.
6 Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?
7 Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu.
8 Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza.
9 Na walipokuja wale wa saa kumi na moja, walipokea kila mtu dinari.
10 Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari.
11 Basi wakiisha kuipokea, wakamnung'unikia mwenye nyumba,
12 wakisema, Hao wa mwisho wametenda kazi saa moja tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na hari za mchana kutwa.
13 Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari?
14 Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.
15 Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema?
16 Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.
Neema ya Mungu yatuokoa;
Yesu anatoa mfano wa wafanyakazi katika shamba la mizabibu walioanza kazi kwa muda tofauti lakini wote wakalipwa ujira sawa, dinari. Wale walioingia wa kwanza kazini walifikiri wangelipwa dinari zaidi, tofauti na wale waliofanya kazi kwa saa moja. Lakini mwenye shamba akawakumbusha kwamba walipatana dinari (13). Mwenye shamba alikazia kwamba ni halali yake kutumia vilivyo vyake apendavyo.
Mstari wa 16 unahitimisha kwamba wa mwisho watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho. Hii inatukumbusha sote kutengeneza njia zetu, maana neema ya Mungu ni kwa wote, haichagui. Mungu hana upendeleo. Uzima wa milele utategemea imani yako na maisha uliyoishi, na siyo muda ulioishi katika wokovu. Hivyo mche Bwana ukatende yote kwa uamininifu, maana Yesu yuaja. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
