Date:
09-02-2026
Reading:
Mwanzo49:9-12
Jumatatu asubuhi tarehe 09.02.2026
Mwanzo 49:9-12
9 Yuda ni mwana-simba, Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke; ni nani atakaye mwamsha?
10 Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.
11 Atafunga punda wake katika mzabibu, Na mwana-punda wake katika mzabibu mzuri. Amefua nguo zake kwa mvinyo, Na mavazi yake kwa damu ya zabibu.
12 Macho yake yatakuwa mekundu kwa mvinyo, Na meno yake yatakuwa meupe kwa maziwa.
Neno la Mungu li hai;
Yakobo aliwapa usia watoto wake kabla ya kufa. Ni usia ambao ukiusoma umejaa baraka. Asubuhi ya leo tumesoma sehemu ya usia huo akimuusia na kumbariki Yuda. Anamtaja Yuda kama mwana Simba kutoka katika mawindo. Yakobo anaendelea kusema kwamba fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, hata atakapokuja yeye mwenye milki, ambaye mataifa watamtii.
Yuda anatofautiana na wenzake kwa kuwa kiongozi katika ardhi iliyokuwa ikimngoja Mesiya. Wakati Rubeni (mzaliwa wa kwanza), Simeoni, na Lawi wakipoteza nafasi zao kwa sababu ya matendo yao, Yuda alitokea kuwa kiongozi wao aliyeonekana kuitunza ahadi ya ujio wa Mesiya.
Mstari wa 10 unamtaja Yuda kuwa kiongozi hadi mtawala atakapokuja, ambaye mataifa watamtii. Kwa mstari huu, unakuja mfuatano wa kiutawala (lineage) kuanzia kwa Yuda mwenyewe, kuja kwa Mfalme Daudi na hatimaye Yesu Kristo. Yesu Kristo ndiye alileta wokovu bure kwa neema, ndiye anatajwa kwenye mstari wa 10 (ambaye mataifa watamtii). Huu ni ushahidi kwamba Yesu ndiye Mwokozi wa ulimwengu tunayepashwa kumwamini na kumfuata. Amina
Uwe na wiki njema
Heri Buberwa
