Date: 
10-02-2026
Reading: 
Mathayo 10:5-15

Jumanne asubuhi tarehe 10.02.2026

Mathayo 10:5-15

5 Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie.

6 Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.

7 Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.

8 Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.

9 Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu;

10 wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake.

11 Na mji wo wote au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata mtakapotoka.

12 Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni.

13 Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi.

14 Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu.

15 Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule.

Neno la Mungu li hai;

Asubuhi ya leo tunasoma Yesu akiwatuma wanafunzi wake kuhubiri Injili. Anawatuma kuwaendea kondoo waliopotea, yaani wale wote ambao hawajamjua na kumwamini yeye (Yesu). Anawatuma kuhubiri wakisema ufalme wa mbinguni umekaribia. Anawatuma kupoza wagonjwa, kufufua wafu, kutakasa wakoma, kutoa pepo. Anawataka kutopokea chochote, kwa uhakika kwamba watapokelewa waendako.

Wanafunzi walikuwa wanapewa wajibu na Yesu, wajibu wa kuhubiri, kufundisha na kuwaombea watu uponyaji. Katika huduma anayowatuma kuifanya, anaanza kuwaambia "...hubirini mkisema ufalme wa mbinguni umekaribia". Matendo mengine ya kuponya wagonjwa na kutakasa wakoma yanakuja baadaye, cha kwanza ni kuhubiri Injili. Msingi wa Kanisa ni Yesu mwenyewe, akitukumbusha kulishika neno lake ili atupe mwisho mwema. Amina

Jumanne njema 

 

Heri Buberwa