Date:
12-02-2026
Reading:
Ezekieli 18:20-22
Alhamisi asubuhi tarehe 12.02.2026
Ezekieli 18:20-22
20 Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake.
21 Lakini mtu mbaya akighairi, na kuacha dhambi zake zote alizozitenda, na kuzishika amri zangu zote, na kutenda yaliyo halali na haki, hakika ataishi, hatakufa.
22 Dhambi zake zote alizozitenda hazitakumbukwa juu yake hata mojawapo; katika haki yake aliyoitenda ataishi.
Neno la Mungu li hai;
Sura ya 18 ya Ezekieli inao ujumbe ulioandikwa kati ya mwaka 593 KK na 571 KK wakati wa uhamisho wa Babeli. Sura iko ndani ya sehemu ya kwanza ya kitabu cha Ezekieli (sura 1-24). Wakati ule iliaminika kwamba kosa la kizazi kimoja linawafuata kizazi kingine, na kuendelea. Kwa hiyo Sura inaelezea uhusiano uliopo kati ya wajibu binafsi na adhabu ya pamoja. Yaani sura inasahihisha msemo ulioandikwa kwenye mstari wa pili ambao ni;
Ezekieli 18:2
Je! Maana yake ni nini hata mkatumia mithali hii katika Israeli, mkisema, Baba wamekula zabibu mbichi, nao watoto wakatiwa ganzi la meno?Msisitizo wa sura hii ni uwajibikaji binafsi kwa sababu ya dhambi na toba. Somo linaanza kwa kusema "Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa, mwana hatauchukua uovu wa babaye...uovu utakuwa juu yake". Ezekieli anatoa habari njema kwamba kwa yeyote atakayetubu dhambi zake hazitakumbukwa, atasamehewa. Neno la Mungu lituongoze kutambua kuwa kila mmoja atawajibika mbele za Mungu yeye peke yake. Mwamini Yesu, timiza wajibu wako, uzima wa milele unatungoja. Amina
Alhamisi njema
Heri Buberwa
