Date:
16-02-2026
Reading:
Mathayo 20:17-19
Jumatatu asubuhi tarehe 16.02.2026
Mathayo 20:17-19
17 Hata Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia,
18 Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi; nao watamhukumu afe;
19 kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeledi, na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka.
Yesu aiendea njia ya mateso Yerusalemu;
Jana ibadani tulisikia habari za Yesu kupanda kwenda Yerusalemu, somo likitoka Mathayo 17:22 lilihusu taarifa hiyo ya kupanda Yerusalemu. Katika Injili za Mathayo, Marko na Luka Yesu alitoa taarifa hii mara tatu. Sasa katika Mathayo, jana tuliona ilikuwa taarifa ya pili. Somo la asubuhi hii ni taarifa ya tatu, ambapo Yesu anawaambia wanafunzi kuwa wanapanda Yerusalemu, huko atahukumiwa afe. Anasema atadhihakiwa, atapigwa mijeledi na kusulibishwa, lakini siku ya tatu atafufuka.
Yesu alikuwa anawaandaa wanafunzi wake kwa mambo yaliyokuwa yanakuja, yaani mateso hadi kufa kwake na kufufuka. Hadi anatoa taarifa moja mara tatu, aliona umuhimu wa kuwaambia hivyo, ili wajue linalokuja. Njia hii aliyoiendea ilimpeleka msalabani hadi kufa na kufufuka. Kumbe njia ya mateso ilikuwa ni kwa ajili ya wokovu wetu. Basi itukumbushe kwamba Yesu ndiye njia ya uzima. Amina
Siku njema
Heri Buberwa Nteboya
