Date:
17-02-2026
Reading:
Warumi 11:25-27
Jumanne asubuhi tarehe 17.02.2026
Warumi 11:25-27
25 Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili.
26 Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake.
27 Na hili ndilo agano langu nao, Nitakapowaondolea dhambi zao.
Yesu aiendea njia ya mateso Yerusalemu;
Ni ujumbe wa Mtume Paulo kwa Warumi, kwamba Israeli wote wataokolewa. Pamoja na ugumu wao, wote wataokoka kwa neema ya Mungu. Paulo anawahakikishia kwamba Yesu aliyekuja duniani alileta wokovu kwa ajili ya watu wote. Anaendelea kuwaambia kwamba Mungu hataangalia walivyomuasi hapo zamani (30). Ni tangazo la rehema.
Mtume Paulo alikuwa anatoa hakikisho la watu wote kuokolewa. Tunapoendelea kutafakari juu ya tangazo la Yesu kupanda Yerusalemu, tunakumbushwa kwamba alikuwa anakwenda kupata mateso, kufa na kufufuka kwa ajili yetu, wote. Kumbe tangazo la wote kuokolewa liko kwetu hata sasa, kwamba kwa Yesu kufa msalabani tumeokolewa. Tudumu katika imani hii maana ndiyo yenye hatma njema ya maisha yetu, yaani uzima wa milele. Amina.
Siku njema
Heri Buberwa
