Date: 
18-02-2026
Reading: 
Yoeli 2:15-20

Hii ni Kwaresma;

Jumatano ya majivu;

18.02.2026

 

Masomo;

Zab 51:1-3; 2 Kor 7:9-10; *Yoe 2:15-20

Yoeli 2:15-20

15 Pigeni tarumbeta katika Sayuni, Takaseni saumu, kusanyeni kusanyiko kuu;

16 Kusanyeni watu, litakaseni kusanyiko, Kusanyeni wazee, kusanyeni watoto, Na hao wanyonyao maziwa; Bwana arusi na atoke chumbani mwake, Na bibi arusi katika hema yake.

17 Hao makuhani, wahudumu wa Bwana, na walie Kati ya patakatifu na madhabahu, Na waseme, Uwaachilie watu wako, Ee Bwana, Wala usiutoe urithi wako upate aibu, Hata mataifa watawale juu yao; Kwani waseme kati ya watu, Yuko wapi Mungu wao?

18 Hapo ndipo Bwana alipoona wivu kwa ajili ya nchi yake, akawahurumia watu wake.

19 Bwana akajibu, akawaambia watu wake; Tazameni, nitawaletea nafaka, na divai, na mafuta, nanyi mtashiba kwa vitu hivyo; wala sitawafanya tena kuwa aibu kati ya mataifa;

20 lakini jeshi lililotoka kaskazini nitaliondolea mbali nanyi, nami nitalifukuza mpaka nchi ya ukame na ukiwa; sehemu yake iliyo mbele itaingia katika bahari ya mashariki, na sehemu yake iliyo nyuma itaingia katika bahari ya magharibi; na uvundo wake utapanda juu, na harufu yake mbaya itapanda juu, kwa sababu ametenda mambo makubwa.

Rarueni mioyo yenu;

Tunapoianza Kwaresma ya mwaka huu tunamsoma Yoeli ambaye anaongelea baraka kwa Israeli, iwapo tu wangetubu. Yoeli ni nabii aliyeongea kwa kurudia sana juu ya toba kwa Israeli, akiwaasa kuacha uovu. Wanazuoni wa Agano la kale hujadili wakati ambao Yoeli aliishi. Kama aliishi kabla au wakati wa uhamisho wa Babeli, basi aliwaonya Israeli kuhusu vita na Ashuru au Babeli, vita ambayo Israeli angepoteza, ilikuwa inakuja. Kama aliishi wakati wa hekalu la pili, anawakumbusha Israeli Agano lao na Mungu. Kwa vyovyote vile, Yoeli anawatahadharisha Israeli kwamba mwisho wa dhambi yoyote ni matokeo mabaya. 

Katika sura ya kwanza, Yoeli anatumia picha ya uvamizi wa nzige kuonesha hatari inayokuja, kwamba hakuna tumaini tena. Soma hapa;

Yoeli 1:4

Yaliyosazwa na tunutu yameliwa na nzige; na yaliyosazwa na nzige yameliwa na parare; na yaliyosazwa na parare yameliwa na madumadu.

Ukiendelea kusoma sura ya 1:13-20, Nabii Yoeli anawaita makuhani na watumishi wa madhabahu kuomboleza kwa sadaka mbele za Mungu. Anawaambia kuita kusanyiko la watu wote, waende mbele za Bwana na kumlilia. Yoeli anaonya kwamba siku ya hukumu inakaribia, hivyo wito wake wa toba kwa Israeli ni halisi. 

Somo lenyewe;

Sasa ukiingia sura ya pili, Yoeli anarejea wito wa toba kama unavyosomeka kwenye 1:13-20. Ingawa usawa huu ukosefu wa tumaini hauonekani, bali Yoeli anaonesha tumaini katika Bwana kwa wote watubuo. Somo linaonesha wito wa kusanyiko la wazee na watoto, maana yake watu wote. Yaani ni kama tulivyo ibadani leo (16). Mstari wa 17 unasisitiza kulia mbele za Bwana, yaani ni wito wa Israeli kwenda mbele za Mungu kwa ibada wakiomba rehema ya Mungu. Mstari wa 18 Yoeli anaonesha huruma ya Mungu kwa wote watubuo. Yaani anawaeleza kwamba wakitubu uhakika ni kusamehewa.

Yoeli anaendelea na unabii wake, mstari wa 19 akionesha Bwana kuwajibu watu wake kwa kuwasamehe dhambi zao. Mstari wa 20 ni hakikisho la kuwashindia vita. Ukiendelea kusoma unaiona ahadi ya Bwana kuhusu nzige tuliowasoma kwenye sura ya kwanza (1:4). Ni ahadi ya kurejesha yaliyoliwa na nzige. Yaani ni ahadi ya kusamehewa dhambi iwapo Israeli wangetubu. Iangalie ahadi hii;

Yoeli 2:25-26

25 Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na nzige, na parare, na madumadu, na tunutu, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu.
26 Nanyi mtakula chakula tele na kushiba, na kulihimidi jina la Bwana, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu; na watu wangu hawatatahayari kamwe.

Rarueni mioyo yenu;

Yoeli aliwaita Israeli kutubu ili wasamehewe kulingana na ahadi ya Bwana, ndilo somo la leo. Baada ya kufa na kufufuka kwa Yesu, Israeli ni wote wamwaminio yeye (Yesu). Kwa hiyo Yesu anatualika kutubu dhambi zetu. Tunapoanza majira haya ya mateso, tunakumbuka Yesu alivyoiendea njia ya mateso, akateseka kwa ajili yetu. Ni wakati tunaokumbushwa kuishi maisha ya toba. Basi tutubu dhambi zetu kama tunavyoalikwa na Kristo mwenyewe, ili atusamehe na kutupa uzima wa milele. Amina

Kwaresma njema

Heri Buberwa Nteboya 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com 

Kwaresma 2026