Date: 
21-02-2026
Reading: 
Yeremia 4:8-9

Jumamosi asubuhi tarehe 21.02.2026

Yeremia 8:4-9

4 Tena utawaambia, Bwana asema hivi, Je! Watu wataanguka, wasisimame tena? Je! Mtu atageuka aende zake, asirudi tena?

5 Mbona, basi, watu hawa wa Yerusalemu wamegeuka waende nyuma, wasikome kugeuka hivyo? Hushika udanganyifu sana, hukataa kurudi.

6 Nalisikiliza nikasikia, lakini walisema yasiyo sawa; hapana mtu aliyetubia maovu yake, akisema, Nimefanya nini? Kila mtu hurudia mwendo wake mwenyewe, kama farasi aendavyo kasi vitani.

7 Naam, koikoi angani ajua nyakati zake zilizoamriwa; na hua na mbayuwayu na korongo huangalia wakati wa kuja kwao; bali watu wangu hawazijui amri za Bwana.

8 Mwasemaje, Sisi tuna akili, na torati ya Bwana tunayo pamoja nasi? Lakini, tazama, kalamu yenye uongo ya waandishi imeifanya kuwa uongo.

9 Wenye hekima wametahayari, wamefadhaika na kushikwa; tazama, wamelikataa neno la Bwana, wana akili gani ndani yao?

Rarueni mioyo yenu;

Yeremia anaangazia upotofu wa Israeli, Taifa ambalo watu wake waligeuka, wakawa na mambo ya udanganyifu, wakasema yasiyo sawa. Lakini katika yote hayo hakuna aliyetubu. Walijiona kuwa na akili kwa sababu walikuwa na torati ya Bwana. Katika yote hayo, Yeremia anawaita kutubu na kurejea kwa Bwana. Yeremia anasema kutotubu ni kulikataa neno la Bwana, na katika hilo anahoji kama wana akili ndani yao!

Ujumbe wa Yeremia wa kutubu kwa Israeli ndiyo unaotujia asubuhi hii. Tutambue kuwa maisha yetu siku zote yanahitaji rehema ya Mungu. Tusilikatae neno la Bwana kama wale anaowasema Yeremia, maana yeye ndiye mwenye kutusamehe na kutupa uzima wa milele. Amina

Siku njema

 

Heri Buberwa