Date: 
28-02-2026
Reading: 
1 Yohana 3:4-9

Hii ni Kwaresma 

Jumamosi asubuhi tarehe 28.02.2026

1 Yohana 3:4-9

4 Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.

5 Nanyi mnajua ya kuwa yeye alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake.

6 Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua.

7 Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki;

8 atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.

9 Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu.

Katika Yesu kila jaribu lina mlango wa kutoka;

Yohana anaandika katika waraka kuhusu dhambi na toba. Anasema kila atendaye dhambi afanya uasi, kwa kuwa dhambi ni uasi. Anakazia kwamba atendaye dhambi ni wa Ibilisi, maana Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Msisitizo wa Yohana ni kwamba kila aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi. 

Kama tulivyosoma, Yohana anasema kila aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, lakini Yohana huyohuyo anasema tukisema hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe;

1 Yohana 1:8-10

8 Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.
9 Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.
10 Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.

Yohana anamaanisha kwamba tujihadhari na dhambi, na tuishi kwa toba kila wakati. Tusitende dhambi, lakini tutubu dhambi kwa sababu sisi ni wenye dhambi. Amina

Siku njema

 

Heri Buberwa