Date: 
06-03-2026
Reading: 
Mathayo 11:28-30

Ijumaa ya tarehe 06.03.2026;

Maombi ya dunia;

Masomo;

Zab 23:2-3; Mwa 2:2-3; *Mt 11:28-30*

Mathayo 11:28-30

28 Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.

"Njooni kwangu, nitawapumzisha"

Utangulizi;

Baada ya kufundisha, kuhubiri na kuponya, wengi waliiamini Injili, lakini wapo ambao hawakuamini. Yaani pamoja na Yesu kutenda ishara kadhaa katikati yao, bado hawakuamini. Ilisababisha Yesu akatoa ole kwa hao ambao hawakuamini na kutubu. Jambo hili linaonekana kwenye Injili tuliyoisoma kabla ya somo la leo, Yesu akitoa ole. Soma hapa chini;

Mathayo 11:21-24

21 Ole wako, Korazini! Ole wako, Bethsaida! Kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika katika Tiro na Sidoni, wangalitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu.
22 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi Tiro na Sidoni kustahimili adhabu zao siku ya hukumu kuliko ninyi.
23 Nawe Kapernaumu, je! Utakuzwa mpaka mbinguni? Utashushwa mpaka kuzimu; kwa kuwa kama miujiza iliyofanyika kwako ingalifanyika katika Sodoma, ungalikuwapo mji huo hata leo.
24 Walakini nawaambieni, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma kustahimili adhabu yake siku ya hukumu kuliko wewe.

Ambao hawakuamini siyo kwamba walikuwa wajinga, hawakuamini kwa sababu zao tu. Torati ilichukua nafasi kwa wengi, bado walikuwa na mioyo migumu. Ndiyo maana ukisoma mstari wa 25 Yesu anamshukuru Baba yake, kwamba mambo haya aliwaficha wenye hekima na akili akawafunulia watoto wachanga. Anaendelea kusema amekabidhiwa vyote, mbinguni na duniani. Hapa Yesu alikuwa anamaanisha watu kumwamini kwa imani, na siyo kwa akili zao.

Somo lenyewe;

Baada ya kutoa "Ole" kwa wasioamini na kutubu, na kuonesha kwamba amepewa vyote mbinguni na duniani, Yesu anatoa wito kwa wote wasumbukao na kulemewa na mizigo ya dhambi, kwa ahadi ya kuwapumzisha. Yesu anaita watu kujitia nira yake na kujifunza kwake, kwa kuwa yeye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo. Huu ni wito wa toba kwa watu wote, yaani Yesu anaita watu kutubu dhambi. Kutubu dhambi siyo jambo la mara moja, bali la kudumu. Yaani maisha ya toba lazima yawe endelevu kwa kila aaminiye. Haimaanishi utende dhambi ili utubu, bali jihadhari na dhambi, lakini utubu kwa sababu sisi ni wenye dhambi.

Leo ni siku ya maombi ya dunia

Maombi haya yanafanyika katika majira haya ya mateso. Ujumbe wa mwaka huu unatukumbusha na kutuita kuja kwa Yesu. Tunaalikwa kutua mizigo yetu kwa Yesu, yaani tutubu dhambi na kurejea kwake. Ni ujumbe unaoendana na ule wa Kwaresma, yaani kutubu na kurejea kwa Bwana. Twende kwa Yesu naye atatupumzisha. Amina

Tunakutakia Ibada njema ya maombi ya dunia. Amina

 

Heri Buberwa Nteboya 

Mlutheri 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com