Date: 
07-03-2026
Reading: 
Yohana 8:1-11

Hii ni Kwaresma;

Jumamosi asubuhi tarehe 07.03.2026

Yohana 8:1-11

1 [Walikwenda kila mtu nyumbani kwake; naye Yesu akaenda mpaka mlima wa Mizeituni.

2 Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha.

3 Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati.

4 Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini.

5 Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje?

6 Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi.

7 Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe.

8 Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi.

9 Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati.

10 Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Je! Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia?

11 Akamwambia, Hakuna, Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.]

Njooni kwangu nitawapumzisha;

Yesu akiwa anafundisha hekaluni, waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi wakimshtaki, kwamba kwa sheria ya Musa alitakiwa kupigwa mawe afe. Pamoja na kumshtaki mwanamke, wao walitafuta sababu ya kumshtaki Yesu. Walipozidi kumhoji akainama na kuandika chini. Waandishi na Mafarisayo walitoka mmoja mmoja wote wakaisha. Inaonekana Yesu alimuandika kila mmoja na dhambi yake, ndiyo maana walitoka mmoja mmoja, wa kwanza hadi wa mwisho. Yesu alipoinuka akamkuta mwanamke peke yake! Akamtangazia msamaha wa dhambi. Tunajifunza nini mwisho wa juma hili?

1. Tusijihesabie haki. Mafarisayo na waandishi walijihesabia haki kwa kumuona mwanamke mzinzi, kumbe nao walikuwa wenye dhambi. Ndiyo maana Yesu alipowaambia asiye na dhambi awe wa kwanza kumpiga mawe waliishia kuondoka mmoja mmoja. Muhimu kufahamu kuwa sisi ni wenye dhambi. Tutubu, tusaidiane, tuombeane.

2. Tunaokolewa kwa neema. Mafarisayo na waandishi walikuja kumshtaki mwanamke mzinzi wakiwa wameishikilia sheria ya Musa ambayo haikuwa na nafasi tena mbele ya Yesu. Ni neema ya Mungu yatuokoa, bure na siyo vinginevyo. Walitakiwa wamlete kwa Yesu aokolewe, na siyo kumshtaki.

3. Yesu anatujua tulivyo. Mafarisayo na waandishi walienda kumshtaki mwanamke mzinzi, walijiona wasafi, Yesu akawaambia dhambi zao! Wakaondoka bila shaka kwa aibu. Yesu anatujua, anatuona, tutubu dhambi zetu.

4. Tutende haki katika jamii yetu. Mwanamke mzinzi alishtakiwa mbele ya Yesu. Huenda ilikuwa sahihi? Huo uzinzi alikuwa anafanya na nani? Mbona aliozini nao hawakuletwa? Haki ilikuwa wapi? Haki iko wapi leo?

5. Yesu anayo mamlaka ya kusamehe dhambi. Mwisho wa tukio la mashtaka ni washtaki kukimbia, na Yesu anamtangazia msamaha wa dhambi yule mwanamke. Turudi kwa Yesu, upo msamaha wa dhambi na wokovu kuelekea uzima wa milele. Amina. Jumamosi njema.

 

Heri Buberwa Nteboya 

 

0784 968650 

bernardina.nyamichwo@gmail.com