Date:
09-03-2026
Reading:
Mwanzo 2:15-17
Hii ni Kwaresma;
Jumatatu asubuhi tarehe 09.03.2026
Mwanzo 2:15-17
15 Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.
16 Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula,
17 walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.
Mazingira ni Uhai tuyatunze;
Kanisa linatuelekeza kutafakari juu ya utunzaji wa mazingira katika juma hili. Katika kumtazama Bwana, kutunza mazingira ni jambo lisiloepukika. Wahubiri wengi tunahubiri sana dhambi nyingine zote mf. wizi, uzinzi, uongo n.k ila suala la utunzaji wa mazingira limesahaulika kabisa. Kitendo cha kuharibu sura ya nchi ni kuharibu uumbaji wa Mungu.
Somo la leo asubuhi tunasoma Mungu akimpa mwanadamu bustani ya Edeni "ailime na kuitunza". Tafsiri yake ni kuwa tumepewa nchi na uzuri wake kuitunza. Uchafuzi wa mazingira una athari kwa viumbe hai tukiwamo sisi binadamu mf magonjwa ya mlipuko. Tuepukane na vitendo vya uchafuzi wa mazingira kama utupaji taka ovyo, kuchafua maeneo tunayoishi, kutiririsha maji machafu, kukata miti ovyo, kuchoma moto mbuga na misitu n.k
Kwa matendo hayo tajwa hapo juu tunaharibu makazi ya binadamu, wanyama na maliasili kwa ujumla. Kwa matendo yote hayo tunatenda dhambi ambazo ni chukizo mbele za Mungu. Macho yetu yamtazame Bwana aliye uzima wetu tukitunza mazingira ili tuufurahie uumbaji wa Mungu. Mazingira ni Uhai tuyatunze. Amina
Uwe na wiki njema ukitunza mazingira
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
