Date:
13-03-2026
Reading:
Mhubiri 11:1-5
Hii ni Kwaresma;
Ijumaa asubuhi tarehe 13.02.2025
Mhubiri 11:1-5
1 Tupa chakula chako usoni pa maji; Maana utakiona baada ya siku nyingi.
2 Uwagawie sehemu watu saba, hata wanane; Maana hujui baa gani litakalokuwa juu ya nchi.
3 Mawingu yakiwa yamejaa mvua, Yataimimina juu ya nchi; Na mti ukianguka kuelekea kusini, au kaskazini, Paangukapo ule mti, papo hapo utalala.
4 Mwenye kuuangalia upepo hatapanda; Naye ayatazamaye mawingu hatavuna.
5 Kama vile wewe usipojua njia ya upepo ni ipi, wala jinsi mifupa ikuavyo tumboni mwake mja mzito; kadhalika huijui kazi ya Mungu, afanyaye mambo yote.
Mazingira ni Uhai tuyatunze;
Sura ya kumi na moja ya kitabu cha Mhubiri huhimiza juu ya ukarimu na kuwekeza katika kazi, kwamba mafanikio ya kweli huja kwa imani na kumwamini Mungu katika bidii ya kazi. Hata pale inapotokea matokeo yakawa kinyume na mategemeo, msisitizo ni kukaa katika Bwana mwenye hatma ya wote wamchao. Sura hii inatumia uoto wa asili kusisitiza kazi, kwa maana ya kutunza uasili wa Mungu kwa maana ya uumbaji.
Somo la asubuhi ya leo linafundisha kufanya kazi kwa kutumia upepo, mawingu na mvua ipasavyo. Ukisogea mstari wa 6 unaelekeza kupanda mbegu asubuhi na jioni. Kwa hiyo ni ujumbe kwamba tufanye kazi kwa bidii. Kumbe tunakumbushwa kuwa tunaishi katika dunia ambayo ni uumbaji wa Mungu, ambamo pamoja na kazi zetu, kuitunza dunia hii ni wajibu wetu. Kutumia mvua, upepo, mawingu na kupanda mbegu leo tunaweza kusema ni kufanya kazi. Kumbe katika kufanya kazi zetu tutunze mazingira. Amina
Ijumaa njema
Heri Buberwa Nteboya
