Hii ni Kwaresma;
Jumatano asubuhi tarehe 01.04.2026
Mathayo 21:1-11
1 Hata walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu alipotuma wanafunzi wawili akiwaambia,
2 Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwana-punda pamoja naye; wafungueni mniletee.
3 Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana anawahitaji; na mara huyo atawapeleka.
4 Haya yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema,
5 Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye amepanda punda, Na mwana-punda, mtoto wa punda.
6 Wale wanafunzi wakaenda zao, wakafanya kama Yesu alivyowaamuru,
7 wakamleta yule punda na mwana-punda, wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake.
8 Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani; na wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani.
9 Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza sauti, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni.
10 Hata alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakisema, Ni nani huyu?
11 Makutano wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya.
Ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana;
Tunaendelea na tafakari ya Yesu kuingia Yerusalemu kwa shangwe. Tukiwa asubuhi ya leo tunairejea Injili ya Mathayo, Yesu anawatuma wanafunzi wawili kwenda kijiji kikichowakabili na kumletea mwanapunda ambaye hajapandwa bado. Yesu aliingia Yerusalemu kwa kumpanda huyo mwana-punda, watu wakiimba Hosana, mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni.
Alipoingia Yerusalemu mji wote ukataharuki! Wapo waliokuwa wanamsubiri kama mkombozi toka kwenye utawala wa Warumi, lakini kumbe Yesu alikuwa anaiendea njia ya mateso kwa ajili ya ulimwengu wote. Tukio hili linatukumbusha njia ya mateso ambayo Yesu aliiendea kutukomboa. Basi tumpokee aingie mioyoni mwetu, tukaishi naye milele. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
