Date: 
07-04-2026
Reading: 
Marko 16:9-11

Hii ni Pasaka;

Jumanne asubuhi tarehe 07.04.2026

Marko 16:9-11

9 Naye alipofufuka alfajiri siku ya kwanza ya juma, alimtokea kwanza Mariamu Magdalene, ambaye kwamba alimtoa pepo saba.

10 Huyo akashika njia akawapasha habari wale waliokuwa pamoja naye, nao wakali wanaomboleza na kulia.

11 Walakini hao waliposikia kama yu hai, naye amemwona, hawakusadiki.

Yesu mfufuka kaa pamoja nasi;

Injili ya Marko inaeleza kwamba Mariamu Magdalene akiwa na Mariamu mamaye Yakobo na Salome walinunua manukato ili wakaupake mwili wa Yesu kaburini. Walipofika kaburini wakakuta jiwe halipo na mwili wa Yesu haupo. Mara wakaona kijana amekaa mkono wa kuume, akawaambia habari za kufufuka kwa Yesu. Ilikuwa ni habari ya mshangao kwao.

Baada ya hapo ndipo somo la leo asubuhi linaonesha Yesu akimtokea Mariamu Magdalene ambaye alikuwa amemtoa pepo saba. Rejea ya Yesu kumtoa Mariamu Magdalene pepo saba hii hapa;

Luka 8:1-2

1 Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu; na wale Thenashara walikuwa pamoja naye,
2 na wanawake kadha wa kadha ambao walikuwa na pepo wabaya na magonjwa wakaponywa; nao ni Mariamu aitwaye Magdalene aliyetokwa na pepo saba,

Huyo ndiye alishika njia kupeleka habari za kufufuka kwa Yesu. Huu ulikuwa uhakika kwa Mariamu Magdalene kwamba Yesu alifufuka. Yesu anawakemea wale kumi na moja kwa kutokuamini kwamba amefufuka maana hawakuwasadiki wale waliomwona alipofufuka. Somo linatupa uhakika kwamba Yesu alifufuka, na kwa sababu hiyo tumpokee mioyoni mwetu akae nasi siku zote za maisha yetu. Amina

Siku njema

 

Heri Buberwa Nteboya