Date:
13-04-2026
Reading:
Yohana 20:3-31
Hii ni Pasaka;
Jumatatu asubuhi tarehe 13.04.2026
Yohana 20:30-31
30 Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki.
31 Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.
Yesu Kristo ajidhihirisha kwa wanafunzi wake;
Yesu alipofufuka alianza kumtokea Mariamu Magdalene, ambaye alikuwa amemtoa pepo saba. Huyu alienda kuwapa wanafunzi habari. Pia aliwatokea wawili kwenda Emau, hawa nao walirudi Yerusalemu kupeleka habari za kufufuka kwa Yesu. Kufufuka kwa Yesu ndiyo ishara kuu inayotajwa katika Injili zote nne (na kulisha watu 5,000).
Lakini pamoja na ishara hiyo ya kufufuka, baada ya kuwatokea Mariamu Magdalene na wale wawili wa kuelekea Emau, Yesu alifanya ishara nyingine, aliwatokea wanafunzi wakiwa wamejifungia ndani! Siku ile alipomtokea Mariamu Magdalene, jioni yake aliwatokea wanafunzi walipokuwa wamejifungia ndani (Yoh 20:19). Aliwatokea tena wakiwa na Thomaso, milango ikiwa imefungwa (Yoh 20:26). Ndiyo, naita ishara maana walijifungia lakini akatokea mbele yao! Kwa hiyo Yesu aliendelea kufanya ishara hata baada ya kufufuka.
Injili ya leo asubuhi hii inasema zipo ishara nyingine nyingi alizofanya Yesu mbele ya wanafunzi wake zisizoandikwa. Lakini hizi chache zimeandikwa ili tupate kuamini kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu. Kwa njia ya neno na ishara Yesu alijidhihirisha kwa wanafunzi wake na wengine wote aliowahubiria na kuwahudumia. Yesu anajidhihirisha kwetu kwa njia ya mahubiri na Sakramenti, akitukumbusha kwamba yeye ndiye Bwana wetu, Mwokozi wa ulimwengu. Amina
Uwe na wiki njema
Heri Buberwa
