Hii ni Pasaka;
Jumanne asubuhi tarehe 14.04.2026
Isaya 25:1-8
1 Ee Bwana, wewe u Mungu wangu; Nitakutukuza na kulihimidi jina lako; Kwa kuwa umetenda mambo ya ajabu, Mashauri ya kale, kwa uaminifu na kweli.
2 Kwa sababu umefanya mji kuwa ni chungu; Mji wenye boma kuwa ni magofu; Jumba la wageni kuwa si mji; Hautajengwa tena milele.
3 Kwa hiyo watu walio hodari watakutukuza, Mji wa mataifa watishao utakuogopa.
4 Maana umekuwa ngome ya maskini, Ngome ya mhitaji katika dhiki yake, Mahali pa kukimbilia wakati wa tufani, Kivuli wakati wa hari; Wakati uvumapo upepo wa watu watishao, Kama dhoruba ipigayo ukuta.
5 Kama vile hari katika mahali pakavu Utaushusha mshindo wa wageni; Kama ilivyo hari kwa kivuli cha wingu, Wimbo wa hao watishao utashushwa.
6 Na katika mlima huu Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa yote karamu ya vitu vinono, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, karamu ya vinono vilivyojaa mafuta, karamu ya divai iliyokaa juu ya urojorojo wake, iliyochujwa sana.
7 Naye katika mlima huu atauharibu uso wa sitara iliyowekwa juu ya watu wote, na utaji ule uliotandwa juu ya mataifa yote.
8 Amemeza mauti hata milele; na Bwana MUNGU atafuta machozi katika nyuso zote; na aibu ya watu wake ataiondoa katika ulimwengu wote; maana Bwana amenena hayo.
Yesu Kristo ajidhihirisha kwa wanafunzi wake;
Kitabu cha Isaya ni kitabu cha unabii katika mpangilio wa vitabu katika Biblia, katika Agano la kale, lakini sio kitabu cha awali cha unabii. Isaya anawekwa wa kwanza kwa sababu unabii wake ni wa kina miongoni vitabu vya kinabii. Kinachotokea katika Isaya, ni kuwa watu wa Mungu wamegawanyika makundi mawili ya ufalme, Israeli upande wa Kaskazini na Yuda upande wa Kusini. Israel amekwishakupata hukumu ya kumkataa Mungu, na Isaya anawasihi watu wa Yuda kumrudia Mungu. Katika sura ya 24, tunaona picha ya hukumu kwa taifa lisilomwabudu Mungu wa kweli.
Kwanza;
Wachambuzi wengi (wa Agano la kale) huwa wanazifanya sura 24 hadi 27 kama sura moja. Sura ya 24 inaanza kwa maneno "Tazama Bwana ameifanya dunia kuwa tupu...." kwamba sura hii inaeleza hukumu ya Mungu juu ya dunia iliyochafuliwa na waliomo, walioasi sheria na kuvunja agano.
Habari ya hukumu inaendelea katika sura ya 25 (somo la leo) inapoonekana Bwana kuufanya mji kuwa chungu, mji wenye boma kuwa magofu, jumba la wageni kuwa sio mji tena, na hautajengwa milele. Lakini pamoja na hukumu hii, mwandishi anamsifu Mungu kwa kutenda mambo ya ajabu (25:1), ambapo Bwana anakuwa kimbilio la maskini, wahitaji na wenye shida mbalimbali (25:4), amejaa tumaini, sio kwa Israeli tu, bali kwa watu wote (25:6)
Sura ya 26 ni wimbo wa ushindi wa kuimbwa katika nchi ya Yuda (26:1) na inaongelea ufufuo;
Isaya 26:19[19]Wafu wako wataishi, maiti zangu zitafufuka; amkeni, kaimbeni, ninyi mnaokaa mavumbini, kwa maana umande wako ni kama umande wa mimea, nayo ardhi itawatoa waliokufa.
Sura ya 27 inaanza kwa ahadi ya Bwana kutoa adhabu;
Isaya 27:1-4
[1]Katika siku hiyo BWANA, kwa upanga wake ulio mkali, ulio mkubwa, ulio na nguvu, atamwadhibu lewiathani, nyoka yule mwepesi, na lewiathani, nyoka yule mwenye kuzonga-zonga; naye atamwua yule joka aliye baharini.Kwa ufupi;
Sura hizi zinataja ushindi wa Bwana juu ya uovu na baraka kwa Israeli na watu wote (25:6)
Somo la leo linaonyesha Mungu kutukuzwa kwa kutenda mambo ya ajabu. Ameukamilisha mpango wake wa wokovu kwa mwanadamu. Mungu alikuwa na mpango na mwanadamu tokea mwanzo alipoitengeneza bustani iliyojaa miti na matunda. Mungu alipanga mwanadamu aifurahie bustani, lakini dhambi ikaondoa hilo. Lakini bado Mungu aliendelea na mpango wa kumkomboa mwanadamu. Huu ni mpango wa zamani sana, toka kuumbwa kwa dunia, mpango ambao ni "amini na hakika". Tunachukua hatua kuuendea wokovu tulioletewa kwa mpango wa Mungu kutukomboa?
Mungu anatukuzwa kwa kuuharibu mji ulioasi. Mji na waliomo, haukuwa na utukufu wa Mungu, na uovu wa mji huu hautatokea tena. Dhana ya mji huu kwa leo, ni dunia tuliyomo. Sisi tulio Taifa la Mungu, tunaitwa kuishi impendezavyo Mungu ili tusiingie hukumuni. Tusiwe mji ulioasi tukaikosa neema ya Mungu.
Sauti ya Isaya ni ya watu waliofunguliwa toka vifungoni. Tafsiri ni kuwa, Mungu alijitambulisha kutunza ahadi zake, katika Imani, watu wakamtambua kuwa ni Mungu. Yesu aliyefufuka ametukomboa, ikiwa ni ahadi ya Mungu kwa wokovu wetu. Tunatambua kuwa tumeokolewa?
Tunaweza kuelewa ukuu wa Mungu, katika maana ya somo hili kwa kuangalia nafasi ya roho. Kuna mawingu, giza na hukumu. Ukuu wa Mungu usioelezeka ni sababu ya kumuamini. Inawezekana tumemfikira Mungu tukaogopa, tukimsikia tunatetemeka, na labda tunafikiri Mungu anatisha!
Mungu ni Upendo.
Upendo wake unatuita kuiendea njia ya msalaba tukitenda mema ili tusiingie hukumuni. Tunapokumbuka ukuu wa Mungu, inatufanya tumsifu. Tunamsifu Mungu kwa hukumu zake, kwa kujiamini kabisa, maana hukumu zake ni za haki.
Ingawaje, inawezekana somo hili kuonyesha ukombozi wa wayahudi, inaenda zaidi kwenye sifa mwa Mungu kwa ushindi wa maadui wa kiroho na faraja kwa wanaomwamini. Imani ya kweli ni ushuhuda kwa Bwana, iendanayo na ukweli kuhusu ahadi zake.
Kwa nyakati za Agano jipya leo; Mungu anatupokea tunapotubu dhambi, na mahali pengine watubuo wanaitwa "mavuno". Waitwao ni wote, wa mataifa na wayahudi. Lipo neno la Mungu, linafariji mioyo na kutia nguvu. Huna haja ya kuishi dhambini, wakati wokovu upo kwa ajili yako.
Katika majira haya ya Pasaka,
Tunakumbushwa kuwa tunawajibika kutenda mema ili tusiingie hukumuni. Tuhakikishe tunaishi kwa kulitii neno la Mungu, tukiwa watu wa toba na msamaha wakati wote, ndipo maisha yetu yatakuwa mapya kila siku, ndani ya Kristo Yesu.
Heri Buberwa Nteboya
0784 968650
