Date: 
21-04-2026
Reading: 
Ezikieli 34:11-19

Hii ni Pasaka;

Jumanne asubuhi tarehe 21.04.2026;

Ezekieli 34:11-19

11 Maana, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo zangu, na kuwaulizia.

12 Kama vile mchungaji atafutavyo kondoo zake, siku ile anapokuwa kati ya kondoo zake waliotawanyika; ndivyo nitakavyowatafuta kondoo zangu; nami nitawaokoa katika mahali pote walipotawanyika, katika siku ya mawingu na giza.

13 Nami nitawatoa katika watu wa mataifa, na kuwakusanya katika nchi zote, nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe; nami nitawalisha juu ya milima ya Israeli, kando ya mifereji ya maji; na katika mahali pote pa nchi panapokaliwa na watu.

14 Nami nitawalisha malisho mema, pa juu ya milima ya mahali palipoinuka pa Israeli litakuwa zizi lao; huko watalala katika zizi jema; nao watakula malisho mema, juu ya milima ya Israeli.

15 Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU.

16 Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu.

17 Na kwa habari zenu, Enyi kundi langu, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nahukumu kati ya mnyama na mnyama, kondoo waume na mbuzi waume pia.

18 Je! Mwaona ya kuwa ni neno dogo ninyi kulishwa malisho mema, hata mkawa hamna budi hukanyaga kwa miguu yenu yaliyosalia? Na kuwa mmekunywa maji yaliyo safi, nanyi hamna budi kuyatibua kwa miguu yaliyobaki?

19 Na kwa habari za kondoo zangu, wao wanakula hayo mliyoyakanyaga kwa miguu yenu, nao wanakunywa maji mliyoyatibua kwa miguu yenu.

Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo;

Nabii Ezekieli anatumia mfano wa Mchungaji kuelezea jinsi viongozi wa Israeli walivyoshindwa kuwaongoza na kuwatunza watu wa Mungu. Viongozi (wachungaji) waliwakandamiza watu (kondoo) kwenye taifa walilopewa na Mungu. Viongozi hawa waliongoza bila kujali watu, walijinufaisha wao kwa maslahi binafsi. Angalia hapa;

Ezekieli 34:2-3

2 Mwanadamu, toa unabii juu ya wachungaji wa Israeli, toa unabii, uwaambie, naam, hao wachungaji, Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao wachungaji wa Israeli, wanaojilisha wenyewe; je! Haiwapasi wachungaji kuwalisha kondoo?
3 Mnawala walionona, mnajivika manyoya, mnawachinja walionona; lakini hamwalishi kondoo.

Somo la leo asubuhi linaonesha Mungu akiahidi kuwatafuta na kuwaokoa kondoo wake. Mungu anatangaza hukumu kwa kondoo wanene (wanufaika na washiriki wa ukandamizaji) lakini pia kuwapa haki yao wanaoonewa. Ni ujumbe unaokuja kwetu kutukumbusha uwajibikaji na kutenda haki kwa mfano wa Yesu Kristo aliye Mchungaji mwema. Amina

Jumanne njema 

 

Heri Buberwa