Hii ni Pentekoste;
Ijumaa asubuhi tarehe 29.05.2026
1 Wakorintho 14:26-33
26 Basi, ndugu, imekuwaje? Mkutanapo pamoja, kila mmoja ana zaburi, ana fundisho, ana ufunuo, ana lugha, ana tafsiri. Mambo yote na yatendeke kwa kusudi la kujenga.
27 Kama mtu akinena kwa lugha, wanene wawili au watatu, si zaidi, tena zamu kwa zamu, na mmoja na afasiri.
28 Lakini asipokuwapo mwenye kufasiri na anyamaze katika kanisa; aseme na nafsi yake tena na Mungu.
29 Na manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue.
30 Lakini mwingine aliyeketi akifunuliwa neno, yule wa kwanza na anyamaze.
31 Kwa maana ninyi nyote mwaweza kuhutubu mmoja mmoja, ili wote wapate kujifunza, na wote wafarijiwe.
32 Na roho za manabii huwatii manabii.
33 Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko, bali wa amani; vile vile kama ilivyo katika makanisa yote ya watakatifu.
Roho Mtakatifu ni nguvu yetu;
Mtume Paulo anawaandikia watu wa Kanisa la Korintho kuhusu ibada yanye utaratibu. Anasema wakutanapo kwa ibada, huduma ya kila mmoja itendeke kwa kusudi la kujenga. Tena hata kuhusu kunena kwa lugha, anasema wanene wawili au watatu tena kwa zamu na mmoja afasiri. Kama hakuna mfasiri, mhusika anyamaze, aseme na nafsi yake na Mungu.
Paulo anakemea watu wawili kuongea kwa pamoja, kwamba aliyeketi akifunuliwa neno, yule wa kwanza anyamaze. Anasema hata manabii wanene wawili, au watatu, na wengine wapambanue. Paulo anasisitiza kwamba inawezekana kila mmoja akawa na uwezo wa kuhutubu ili wote wapate kujifunza na kufarijiwa. Anahitimisha kwamba Mungu si wa machafuko, bali wa amani.
Mtume Paulo anatukumbusha kutii utaratibu tuliokubaliana kwenye ibada. Kanisa letu linao utaratibu wa Liturjia, uheshimike. Kuongeza vionjo na mbwembwe kinyume na makubaliano ni kukosa nidhamu, ni kiburi, dharau na kutokujielewa. Pentekoste ya mwaka huu itukumbushe kuheshimu taratibu za ibada zetu. Kelele zinazopigiwa chapuo kwa kisingizio cha Roho Mtakatifu wakati mmojawapo akipiga makofi huyo roho anapotea ni uhuni. Mliopewa mamlaka sharikani na mitaani simamieni taratibu za ibada zetu, maana kama Paulo anavyosema, Mungu wetu ni wa utaratibu. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
