Date: 
03-06-2026
Reading: 
Nehemia 4:16-20

Jumatano asubuhi tarehe 03.06.2026

Nehemia 4:16-20

16 Ikawa tokea wakati huo, nusu ya watumishi wangu walitumika katika kazi hiyo, na nusu yao wakaishika mikuki, na ngao, na pinde, na darii; na maakida walikuwa nyuma ya nyumba yote ya Yuda.

17 Watu wale walioujenga ukuta, na wale waliochukua mizigo, walijitweka wenyewe, kila mtu alifanya kazi kwa mkono mmoja, na kwa mkono wake wa pili alishika silaha yake;

18 nao wajenzi, kila mtu alikuwa na upanga wake, umefungwa ubavuni mwake, ndivyo alivyojenga. Na yeye aliyepiga baragumu alikuwa karibu na mimi.

19 Nikawaambia wakuu, na mashehe na watu wengine; Kazi hii ni nyingi, tena kubwa, nasi tumetawanyika juu ya ukuta, kila mtu mbali na mwenzake;

20 basi mahali po pote mtakaposikia sauti ya baragumu, enendeni huko, mkatujie; Mungu wetu atatupigania.

Mungu mmoja; Baba, Mwana na Roho Mtakatifu;

Ndugu wakae pamoja kwa umoja;

Jana asubuhi tuliona Nehemia alivyopambana na kundi ambalo halikutaka ukuta wa Yerusalemu kujengwa tena. Katika kupambana huko alitanguliza imani kwa kumuomba Bwana. Imani yake iliendana na matendo, akaweza walinzi kuzunguka eneo la ujenzi ili lisivamiwe. Yaani aliomba, halafu akatimiza wajibu wake.

Somo la asubuhi hii linaonesha ukuta ukilindwa, wajenzi wakiendelea na kazi kila mmoja akiwa na upanga. Katika yote hayo walimtegemea Bwana. Nehemia anahitimisha kwa tegemeo kwamba "Mungu wetu atatupigania". Nasi tuendelee kuwa na imani tukiamini kwamba "Mungu wetu atatupigania". Amina

Siku njema

Heri Buberwa