Ijumaa asubuhi tarehe 05.06.2026
Ezra 1:5-11
5 Ndipo wakaondoka wakuu wa mbari za mababa, wa Yuda na Benyamini, na makuhani, na Walawi, naam, watu wote ambao Mungu amewaamsha roho zao kukwea, ili kuijenga nyumba ya Bwana, iliyoko Yerusalemu.
6 Na watu wote waliokaa karibu nao pande zote wakawatia nguvu mikono yao, kwa vyombo vya fedha, kwa dhahabu, kwa mali, na kwa wanyama, na vitu vya thamani, zaidi ya vile vilivyotolewa kwa hiari ya mtu.
7 Tena Koreshi, mfalme, alivitoa vyombo vya nyumba ya Bwana, alivyokuwa amevileta Nebukadreza toka Yerusalemu ,na kuvitia katika nyumba ya miungu yake.
8 Naam, vyombo vile ndivyo alivyovitoa Koreshi, mfalme wa Uajemi, kwa mkono wa Mithredathi, mtunza hazina; naye akavihesabu mbele ya Sheshbaza, mkuu wa Yuda.
9 Na hii ndiyo hesabu yake; sinia za dhahabu thelathini, sinia za fedha elfu, visu ishirini na kenda.
10 mabakuli ya dhahabu thelathini, mabakuli ya fedha ya namna ya pili mia nne na kumi, na vyombo vingine elfu.
11 Vyombo vyote vya dhahabu na vya fedha vilikuwa jumla yake elfu tano na mia nne. Hivyo vyote Sheshbaza akakwea navyo, hapo walipokwea wale wa uhamisho kutoka Babeli mpaka Yerusalemu.
Ndugu wakae pamoja kwa umoja;
Ezra katika sura ya kwanza anaandika kuhusu mwisho wa uhamisho wa Babeli. Ni maelezo jinsi Mungu alivyoiamsha roho ya mfalme Koreshi wa Uajemi kutoa amri ya kuwaruhusu Wayahudi kurudi Yerusalemu na kujenga upya hekalu. Katika kutimiza unabii wa Yeremia, Mungu anamuongoza Koreshi kutangaza uhuru kwa Israeli waliokuwa uhamishoni.
Koreshi siyo kwamba tu aliwaruhusu Israeli kurudi Yerusalemu, bali aliamuru wasaidiwe gharama za safari na kujenga hekalu. Somo linaonesha Israeli wakiondoka kurejea Yerusalemu, wakipata msaada wa kifedha. Koreshi mwenyewe alitoa vyombo vya nyumba ya Bwana alivyokuwa amevileta Nebukadreza toka Yerusalemu na kuvitia katika miungu yake, akawarejeshea warudi navyo.
Ni historia inayotukumbusha Mungu alivyowarudisha Israeli kutoka uhamishoni Babeli kurudi Yerusalemu. Hakuwaacha, unabii wa Yeremia ukatimia. Historia hii inaonesha kwamba Mungu hawaachi watu wake. Nasi hajatuacha, tuendelee kumtegemea daima katika maisha yetu ya kila siku tukimtumikia kwa uaminifu hata kufa. Amina
Siku njema
Heri Buberwa Nteboya
