Date: 
08-06-2026
Reading: 
Mwanzo 17:15-19

Jumatatu asubuhi 08.06.2026

Mwanzo 17:15-19

15 Mungu akamwambia Ibrahimu, Sarai mkeo, hutamwita jina lake Sarai, kwa kuwa jina lake litakuwa Sara.

16 Nami nitambariki, na tena nitakupa mwana kwake, naam, nitambariki, naye atakuwa mama wa mataifa, na wafalme wa kabila za watu watatoka kwake.

17 Ndipo Ibrahimu akaanguka kifudifudi akacheka, akasema moyoni, Je! Mtu wa umri wa miaka mia, kwake atazaliwa mtoto? Naye Sara mwenye umri wa miaka tisini atazaa?

18 Ibrahimu akamwambia Mungu, Lau kwamba Ishmaeli angeishi mbele yako.

19 Mungu akasema, Sivyo, lakini Sara mkeo atakuzalia mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake Isaka. Nami nitafanya agano langu imara kwake kuwa agano la milele kwa ajili ya uzao wake baada yake.

Kumtegemea Mungu ni maandalizi ya maisha yajayo;

Baada ya Mungu kumbadili jina Abramu na kumfanya Ibrahimu, pia Sarai kuwa Sara, anaweka agano. Katika Agano hilo anasema atambariki Sara kuwa mama wa mataifa mengi. Ibrahimu mwenyewe alianguka na kucheka, maana hakuamini mwanamke mwenye miaka tisini kama Sara alivyokuwa kuzaa! Ukipewa leo taarifa kama hiyo utaamini? 

Lakini Mungu anamwambia Ibrahimu kwamba Sara atakuzalia mtoto wa kiume, na utamwita Isaka. Ujumbe wa asubuhi ya leo unatokana na kitendo cha Ibrahimu kucheka kwa kutokuamini kwamba Sara angepata mtoto uzeeni. Lakini Ibrahimu aliambiwa kuamini atapewa mtoto. Kwa sisi wa Agano jipya, tunakumbushwa kumtegemea Mungu katika maisha yetu, na kumtanguliza katika yote. Hajawahi kutuacha, hiyo ndiyo ahadi yake. Mwamini sasa uokolewe. Amina

Uwe na wiki njema

 

Heri Buberwa