Jumatano asubuhi 10.06.2026;
Mathayo 19:23-30
23 Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni.
24 Nawaambia tena, Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.
25 Wanafunzi waliposikia, walishangaa mno, wakisema, Ni nani basi awezaye kuokoka?
26 Yesu akawakazia macho, akawaambia, Kwa wanadamu hilo haliwezekani; bali kwa Mungu yote yawezekana.
27 Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?
28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.
29 Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele.
30 Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.
Kumtegemea Mungu ni maandalizi ya maisha yajayo;
Kijana mmoja alimfuata Yesu akamuuliza afanye nini ili aurithi uzima wa milele. Yesu akamjibu kwamba azishike amri kama ilivyoandikwa tangu kale, yaani Usiue, usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, waheshimu baba yako na mama yako, na mpende jirani yako kama nafsi yako (Mt 19:18-19)
Yule kijana alimwambia Yesu kuwa hayo alikuwa ameyashika tangu utoto wake. Yesu akamwambia akauze vyote alivyokuwa navyo awape maskini. Kijana aliondoka na huzuni, maana alikuwa na mali nyingi.
Somo linaanzia hapo;
Yesu ndipo anasema kwamba itakuwa vigumu kwa tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu. Wanafunzi walishangaa wakiona haiwezekani kuokoka sasa. Lakini Yesu aliwatia moyo, kwamba wataketi naye mbinguni wakidumu katika kumfuata yeye. Anatoa ahadi ya uzima wa milele kwa watakaomfuata milele. Nasi tukimfuata Yesu daima tutaurithi uzima wa milele. Amina
Siku njema
Heri Buberwa
